Je, unahitaji Kuokoka?
“Ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana na
kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.”
Inawezekana kabisa ya kuwa wewe unayesoma ujumbe huu hujaokoka- yaani hujampokea Yesu Kristo ndani ya moyo wako; kama Bwana na Mwokozi wako, lakini sasa umeona umuhimu wa kumpokea Yesu Kristo katika Maisha yako.
Kwa hiyo kama unataka kuokoka – tafuta mahali palipo
na utulivu, na usome kwa sauti sala ifuatayo: (ukiweza unaweza kupiga magoti
unapoomba sala hii)
SALA YA TOBA
Ee Mungu wangu ulie Mtakatifu. Ninakuja mbele zako. Mimi ni mwenye dhambi. Naomba unisamehe dhambi zangu zote nilizokukosea katika maisha yangu. Ninatubu kweli. Naomba damu ya Yesu Kristo iliyomwagika msalabani kwa ajili yangu initakase sasa katika roho yangu na nafsi yangu na mwili wangu. Nimefungua moyo wangu. Bwana Yesu Kristo nakukaribisha ndani yangu. Ingia kwa uwezo wa Roho wako – uwe Bwana na Mwokozi wangu kuanzia sasa na siku zote. Ahsante kwa kunisamehe na kwa kuniokoa. Nimejitoa kwako nikutumikie katika siku zote za maisha yangu. Shetani hana mamlaka tena juu yangu katika jina la Yesu Kristo. Amina.
HONGERA KWA KUOKOKA
Ikiwa umesoma sala hii kwa kukusudia kabisa na kwa imani, basi wewe umeokoka na dhambi zako zimesamehewa na kusahauliwa na Mungu sawasawa na alivyoandika katika neno lake. Damu ya Yesu iko juu yako sasa.
Baada ya kuokoka
Unapoanza maisha haya mapya katika Yesu Kristo
nakushauri mambo yafuatayo:
1. Zungumza na Mungu kwa maombi kila siku (Yohana 15:7)
2. Soma Neno la Mungu (Biblia) kila siku (Matendo ya Mitume 17:11)
3. Mruhusu Roho Mtakatifu akutawale (Wagalatia 5:16-25; Warumi 8:14-17)
4. Umtumaini Mungu kwa kila jambo katika maisha yako (1Petro 5:7; Zekaria 4:6)
5. Usiache kukusanyika na kushirikiana na wengine waliompokea Yesu Kristo kuwa
Mwokozi wao kama wewe ili uimarike zaidi (Waebrania 10:25)