Mradi wa Watoto Yatima na Watoto walio na maisha magumu - Nsalaga

Historia na Chimbuko

Kituo cha Nsalaga kilianza mwaka 2006, baada ya kanisa kuona matatizo ya watoto yatima na Watoto wenye maisha magumu (OVC) huko Mbeya. Familia nyingi ni maskini sana zenye mtu mzima mmoja na watoto kadhaa. Baadhi ya waangalizi ni wagonjwa au wana VVU na wanategemea sana msaada wa watoto wao.

Tatizo kubwa lingine ni elimu. Katika shule ya msingi mahitaji mengi yanahitajika (sare, vifaa). Malipo mengi ya ziada huongezwa; hasa katika darasa la 7 masomo ya ziada ambayo ni muhimu kwa maandalizi ya mitihani na matokeo bora. Watunzaji hawana chanzo maalumu cha kipato – hivyo, wanafanya biashara ndogo ndogo ili wapate pesa. Ndiyo maana, mradi huu unasaidia familia hizi kwa kulipa ada za shule, vifaa vya shule na sare.

Kituo kinapatikana Nsalaga, Uyole, ambapo kanisa lina ardhi kubwa. Watoto wanakaa na walezi wao na wanatembelewa na wanaojitolea kila mwezi. Kila Jumamosi kuna program kituoni, ambapo watoto hupata msaada wa kisaikolojia, chakula, masomo ya ziada na wanafundishwa Biblia.

Mwaka 2014, vituo viwili vilifunguliwa, maeneo ya vijijini mkoani Mbeya ambayo ni Ilindi na Chunya. Watoto hupata msaada sawa na watoto wa Nsalaga, lakini hukutana mara mbili kwa mwezi kwa sababu wanaishi mbali.

Mradi upo chini ya idara ya wanawake na watoto na ulianza na watoto 45. Kwa sasa jumla ya watoto wapatao 350 wanasaidiwa katika maeneo matatu yote. Tangu kituo kianzishwe, zaidi ya watoto 568 wamesaidiwa.

Malengo

Lengo kuu ni kuboresha maisha ya watoto yatima na watoto walio na mazingira magumu. Matokeo ya baadaye, tunataka kuhakikisha

  1.  kwamba mahitaji ya elimu ya msingi na ya sekondari yanapatikana, ni uwekezaji muhimu kwa kutimiza ndoto za watoto
  2. kwamba kuna muda wa kutosha wa kutoa ushauri na msaada wa kisaikolojia katika jamii
  3. kwamba watoto watapata huduma za msingi za kiafya.
  4. kwamba kituo kinakua na kuendesha shughuli kadhaa wakati wa mchana kwa wiki
  5. kwamba suala la maambukizi ya VVU / UKIMWI linatibiwa
  6. kwamba watoto wanapata mafunzo ya ujuzi wa maisha

Kutokana na malengo hapo juu yanapelekea shughuli zifuatazo:

 a. Elimu

  • Kutoa msaada wa kutosha kwa elimu ya msingi na ya sekondari, na mafunzo ya ufundi kwa kusaidia ada, sare, na vifaa vya shule.
  • Kuinua ufaulu wa kitaaluma wa wanafunzi, yaani kwa kutoa masomo ya ziada shuleni kwa darasa la 7, kidato cha  2 na  cha 4 na kwa kuwapa mazoezi ya kufanya.

 b. Ushauri na msaada wa kisaikolojia katika jamii

  • Kuhakikisha kwamba kila mtoto angalau kwa mwezi anatembelewa nyumbani na mtu anayejitolea anayeishi karibu.
  • Kuhakikisha kwamba ushauri unatolewa kituoni, kwa kuweka masaa ya ushauri

  • Kutoa msaada wa kisaikolojia kupitia shughuli na mbinu rafiki (kwa mfano, masomo ya Biblia, klabu ya watoto, kazi zinazohusu kumbukumbu, usimulizi wa hadithi, haki za watoto na unyanyasaji wa watoto.


 c. Afya

  • Kutoa chakula chenye lishe na maji safi siku ambazo kituo kinafunguliwa

  • Usajili wa watoto wote katika CHF (bima ya afya)

  • Uchunguzi wa mara kwa mara wa afya za watoto hapo kituoni (2-3 kwa mwaka)

  • Kuwafundisha watoto usafi na kuwapa vitendea kazi muhimu

 d. Shughuli baada ya vipindi vya darasani

  • Michezo

  • Uchoraji, uimbaji, na maigizo

 e. Maambukizi ya VVU / UKIMWI

  • Kutoa ushauri nasaha na upimaji  VVU kwa watoto

  • Kuelimisha njia za kuzuia maambukizi ya VVU / UKIMWI kupitia elimu ya kijinsia na kuelimisha juu ya unyanyasaji wa kijinsia kwa vijana

 f. Mafunzo ya stadi za maisha

  • Kufundisha kuhusu unyanyasaji wa watoto na haki za watoto

  • kufundisha kuhusu shughuli za kuzalisha kipato kama vile upandaji, kulima bustani, kufuga kuku, ufugaji na ujasiriamali

Lengo la kituo hiki ni kuwasaidia watoto wajitegemee hapo baadaye kwa kupata elimu na kujifunza kuhusu stadi za maisha vituoni.

Kama ilivyoelezwa katika historia ya mradi, kanisa lilichukua hatua ya kusaidia watoto wenye mahitaji makubwa. Kuhusiana na hali ya baadaye ya Nsalaga ndani ya kanisa hali inaonekana kuimarisha kituo na kupanua huduma na shughuli zake. Hii itakuwa sambamba na shughuli za kuzalisha kipato Nsagala.

Uendelevu

Elimu

Kuna maeneo mbali mbali ambayo kazi endelevu zimefanyika. Kadiri bajeti inavyoruhusu, wanafunzi wote wanapokea msaada kwa ajili ya shule. Kabla au muda mfupi baada ya mwanzo wa mwaka mpya wa masomo au muhula, wanafunzi wanaohitaji msaada, wanawasilisha mahitaji yao kwa kiongozi au mmoja wa wanaojitolea. Watoto wanasaidiwa kuanzia shule ya msingi hadi Chuo Kikuu. Wanafunzi wasiofaulu mitihani yao wanaweza kufanya mafunzo ya miaka 2 katika vituo vya mafunzo ya ufundi kama vile MVTC, VETA, Kakozi. Hii itawawezesha kuanza biashara mapema na kujitegemea wakiwa watu wazima. Wakiweza kujitunza wenyewe, itakuwa faida kwa jamii.

Afya na Chakula

Mradi unahakikisha kwamba watoto wanaosaidiwa wanapata chakula wanapokuja vituoni. Chakula chao kinazalishwa katika Nsalaga, kinachopandwa na kuvunwa na watoto wa kituo hicho. Chakula kinaandaliwa na watoto wenyewe. Hivyo, wanajifunza ujuzi wa maisha.

Watoto hupewa mahitaji ya kupeleka nyumbani; kama vile mchele, sabuni, sukari, chumvi, miswaki, dawa za meno n.k. Familia zinazoongozwa na watoto wanapata msaada zaidi. Hii ni muhimu kwa sababu wasingekuwa na chakula cha kutosha, ingeathiri uwezo wao wa kujifunza vizuri.

Msaada wa kisaikolojia

Watoto wanapata fursa ya kubadilishana mawazo juu ya jitihada wanazozifanya wanapokutana kituoni au wakati watu wanaojitolea wanapofanya ziara za nyumbani. Watoto wanaohudhuria vituoni hupokea mafunzo stadi ya maisha, mafundisho ya Biblia na kupata fursa ya kukutana. Hii huwasaidia kujiamini, kutoa maamuzi sahihi na kujitegemea.

Wafadhili

Wafadhili wakuu ni:

  • Washarika  ndani ya jimbo

  • Waumini nje ya Kanisa la Moravian

  • Rafiki wa kanisa kutoka nje ya nchi: Mission 21, kanisa mji wa Muehlacker, HMH

Wanufaika

Kundi lengwa ni watoto walio na mazingira magumu zaidi. Wengi wao ni yatima; watoto waliopoteza mzazi mmoja au wawili. Baadhi ya watoto wanaishi na mmoja wa wazazi (katika kesi nyingi wanaishi na mama), babu na bibi (mara nyingi pamoja na bibi) au ndugu kama vile shangazi au wajomba. Wachache  wanaoishi wenyewe pamoja na kaka zao na dada zao.

Pia, waangalizi wao watafaidika na msaada kuhusiana na matunzo na, baadaye, kutoka Elimu ya Sekondari ya mtoto. Kwa muda mrefu, jamii nzima itafaidika.


Kiongozi wa mradi Bahati Mshani (katikati) na viongozi wasaidizi wa mradi Phoebe (kushoto) na Silja Riedmann (kulia)
Mawasiliano

Kanisa la Moravian Tanzania - Jimbo la Kusini Magharibi
Mradi wa Watoto Yatima na Watoto walio na maisha magumu - Nsalaga


P.O. Box 377
Mbeya
Tanzania

Simu:    +255 753 024751
Barua Pepe:   bahatimshani@yahoo.co.uk



Kiswahili